Sehemu Ya (139) : Madhara Ya Kuwaachia Ndugu Washikilie "Mahusiano Yako / Ndoa Yako"
UHUSIANO wowote unajengwa na upendo, uaminifu na msamaha. Kila mtu
anapaswa kumpenda mwenzake, kumthamini na kumjali. Hii haishii hapo,
ukishampenda na kumthamini, unapaswa kuwa mwaminifu kwake.
Usipokuwa mwaminifu, maisha ya uhusiano hayawezi kuwa na uhai. Hakuna
mtu anayeweza kufurahia kusalitiwa. Usaliti unauma hivyo ni vyema kila mtu
akaepuka usaliti. Si mwanaume wala mwanamke, hakuna mwenye kibali cha usaliti.
Usaliti unaharibu uhusiano. Usaliti unabomoa ndoa. Wanandoa wanapaswa
kutosaliti kabisa. Kama hiyo haitoshi, ili waweze kudumisha amani ndani ya
nyumba, kila mmoja wao anapaswa kujua kusamehe.
Kila binadamu ana upungufu. Hakuna aliyekamilika hivyo inapotokea
mmekwaruzana ndani ya nyumba, ni vyema mkaombana msamaha. Anayeomba msamaha,
aombe kwa dhati na wewe unayeombwa, basi uwe tayari kusamehe kutoka moyoni.
Mkisameheana, mkachukuliana udhaifu, hakika hakuna kitakachowashinda.
Kila mmoja abebe udhaifu wa mwenzake, aone kwamba hajakamilika na anahitaji
kufanyia kazi udhaifu wake kwa muda fulani ili aweze kubadilika.
Marafiki zangu, maisha ya ndoa yanahitaji usiri. Kila mmoja wenu hawe
na kifua cha kuhifadhi mambo. Ndoa ni taasisi ambayo wenye haki miliki ya ndoa
hiyo ni ninyi wawili. Kila mmoja kwa nafasi yake, ana wajibu wa kutimiza
majukumu yake ili muweze kufika salama.
Asiwepo hata mmoja wa kumdharau mwenzake. Kila mmoja amuone mwenzake
ana umuhimu katika kuhakikisha mnafikia kwenye hatua ya mafanikio ambayo ninyi
wawili mtakuwa mmepanga kuifikia. Iwe ndani ya mwaka mmoja au miaka kadhaa.
Jamani kuna madhara makubwa sana katika ndoa endapo tu utaruhusu ndoa
yako ishikiliwe na ndugu. Ndugu wanapaswa kuwa na nafasi yao katika familia
yenu, lakini wawe na mipaka.
Kuna mambo ambayo mnatakiwa kuyashughulikia ninyi wenyewe.
Hata kama ni ushauri, inashauriwa uombe kwa wale waliokuzidi umri,
lakini bado unaambiwa akili za kuambiwa changanya na zako. Sikiliza ushauri wa
ndugu, lakini jukumu la kufanya uamuzi liwe la kwako.
Unapokuwa kila jambo unalipeleka kwa ndugu, unawapa nafasi kuwa waamuzi
wa ndoa yenu.
Ndugu wanakuwa wanawajua vizuri kuliko hata mnavyojijua ninyi wenyewe,
hilo ni tatizo. Mathalani mmegombana, kabla ya kufika kwa ndugu, hakikisheni
mnalishughulikia ninyi wenyewe kwanza.
Msiwe wepesi wa kupeleka tatizo la ugomvi wenu kwa wazazi. Litatueni
ninyi wenyewe kwa kufuata misingi ambayo mlifundishwa na wazazi wenu wakati
kila mmoja alikuwa akiishi kwao.
Madhara ya kuwashirikisha ndugu hufika mahali wao ndiyo wanageuka
wapangaji wa mambo yenu.
Watawapangia matumizi, watawapangia miradi mnayopaswa kuifanya na
kuwataka muache miradi fulani kutokana na matakwa yao, hiyo ni hatari.
Watawatoa kwenye mstari wenu ambao mnapaswa wenyewe kujiamulia.
Wanandoa ndiyo madereva wa ndoa. Ninyi ndiyo mnashauriana kwa hoja. Mke
aweke hoja zake mezani, mume naye azisikilize na mwisho wa siku muwe na jibu la
pamoja. Mume naye aje na hoja zake, mke azisikilize, ashauri na kuboresha na
mwisho wa siku mnaamua kwa pamoja.
Jambo mtakaloamua ninyi wawili, ndilo litakuwa dira yenu. Ndilo
litakalokuwa kama katiba au sheria ya maisha yenu. Asiwepo mtu wa kuwakosoa au
kuwataka muishi kama fulani anavyoishi. Ninyi mbaki kuwa ninyi na kama
mtapatia, watakuja kuwapongeza baadaye.
Hata ikitokea mmekosea, msikate tamaa. Hayo ni maisha yenu na kama bado
mnapumua, mna nafasi nyingine ya kuboresha safari yenu. Mnaruhusiwa kujifunza
mazuri kupitia wenzenu, lakini lazima mchuje, mlitafakari kwa pamoja na kutoka
na jibu lenu.
Mtakaloamua ndilo lenu. Ukiruhusu sana ndugu waingilie ndoa yenu,
wanaweza hata kuwashauri muachane maana wao hawajui thamani ya penzi lenu. Ni
rahisi tu kuwaambia; ‘achana naye bwana.
Watumiaji Wa "Android" Unaweza Download App Yangu Hapo Chini
Pia Unaweza Nifollow:
Facebook , Instagram , Snapchat , Twitter @KissToTheLadies
WhatsApp +255 715 758 021
Post a Comment